WALIOSHIRIKI katika uchaguzi mkuu uliopita (2010) pamoja na mambo mengine wameona jinsi nchi yetu ilivyo kubwa na ugumu wa kufika kila mahala. Sehemu ambazo
wagombea wengi waliweza kufika ilikuwa ni kijisehemu tu cha nchi. Na hawa ni wale waliotumia pia helikopta, wenzao waliishia kufikia katika wilaya mbili au tatu tu nchini.
Halafu jaribu kuona uwezekano wa serikali iliyoko Dar es Salaam au Dodoma kufanikisha kupanga, maamuzi, kutekeleza na kudhibiti mambo yanayoendelea huko Mara, Ruvuma au Njoluma! Kazi kweli.
Baada ya hapo, angalia kwa karibu sana, idadi ya wapiga kura Zanzibar (waliomchagua rais, bunge/baraza lao na kisha mawaziri wao ni chini ya laki nne ) na wapiga kura wa mikoa ya Tanzania bara. Halafu oanisha hili la kuwa na mkuu wa mkoa (asiyechaguliwa) na mkuu wa wilaya (asiyechaguliwa) na kisha viongozi wa serikali za mitaa, mamenya na madiwani wa kuchomekewa. Na kisha jiulize, je, mikoa inayoendeshwa kwa mfumo huu uliochakaa, uliochujuka na unaovuja kushoto na kulia kama kweli unaweza kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi mikoani.
Ukikaa na kuwaza na kisha kuondoa hofu zinazopandikizwa mioyoni mwetu na viongozi waliochoka kazi na wasioweza kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii, ninaamini utakachoshusha pumzi na kukisema ni kuwa;
' Mikoa huru inayojiendesha kama nchi ndogo ndani ya nchi kubwa, na kila mkoa ukiwa na Waziri wake Mkuu, mawaziri na wabunge wa bunge la chini ndio njia pekee ya kunusuru watu wetu na kasi ya maendeleo ambayo haipishani sana na kasi ya kinyonga...'
Ajabu ya Tanzania ni ile ya kuwa na eneo linaloitwa Zanzibar lenye wapiga kura wasofikia hata laki nne (400,000) na mwaka huu 2010 wapiga kura wake walikuwa kama laki tatu na nusu tu (350,000) lakini eneo hilo la nchi lina rais na mawaziri wake.
Huko bara kuna mikoa na hata majimbo yenye wapiga kura kama hao au maradufu ya hao, lakini maeneo hayo hayafikirii kuwa na kiongozi kama waziri mkuu au gavana na idadi ya mawaziri wake ambao kwa umoja wao wanaweza wakabadili kabisa mustakabali wa kimaendeleo wa maeneo husika.
Kikatiba, tayari hapa kuna tatizo la kiuwakilishi nalo sio lingine ila lile la wapiga kura laki tatu kuwa na rais, makamu wa pili wa rais, baraza la mawaziri na bunge lake, lakini maeneo yenye mamilioni ya wapiga kura halina haki ya namna hii. Haibadilishi kitu hata kama eneo hilo lenye watu wachache linaitwa nchi na lenye watu wengi linaitwa mkoa fulani.
Huko tunakokwenda ili kuendelea maamuzi yafapaswa kufanya kwa kasi ya kupiga simu ya mkononi, utekelezaji kwa spidi ya kutuma ujumbe mfupi na udhibiti kwa kasi ya kutia tiki kwenye viboksi fulani kwenye ujumbe wa simu ya mkononi papo kwa hapo. Matatizo ya wananchi hayastahili kuwa wagonjwa kwenye sehemu ya mapokezi wakisubiri zamu yao ifike, ili daktari toka Dar es Salaam awaone na kuwapiga tarehe. Matatizo mikoani yanahitaji kuwa katika mchakato wa kila siku wa maisha ya mkoa husika. Fursa zilizopo ndani ya mkoa; kati ya mkoa mmoja na jirani zake na kati ya mkoa na nch jirani haziwezi kuguswa zikausaidia mkoa kwa mfumo tulio nao bali kwa kuwa na mikoa ambayo ina viongozi wenye uwezo wa kuamua na kutekeleza papo kwa hapo masuala yote yanayoweza kunufaisha wakazi wake na nchi nzima na hususan yale ya kiuchumi na kijamii.
Fikra hizi zinakuja wakati ambapo tayari kuna ushahidi tosha kwamba hata viongozi wa juu wa kitaifa wakiwa wazuri namna gani kama viongozi wa mashina, yaani, vijiji, wilaya na mkoa hawatatokana na ridhaa ya wananchi wao na hawatakuwa wazuri ni muhali maendeleo ya kweli kupatikana.
Katika kampeni za mwaka huu na wakati wa uchaguzi mkuu 2010 pamoja na mchakato mzima wa utoaji matokeo kwa kila kituo, jimbo, wilaya na mkoa imeonekana dhahiri kuwa Tanzania ni kubwa mno na haifai kuendelea kutawaliwa kijiografia, kisiasa, kiuchumi na kijamii kutokea eneo moja kama vile Dar es Salaam au Dodoma.
Matatizo yanayotokea pale Tanzania inapotawaliwa kutokea Dar es salaam (ambayo ndio makao makuu ya kweli ya nchi hivi leo) ni kama yafuatayo:
. Maamuzi kutokea Dar es salaam yanachukua muda mrefu kutekelezwa katika ngazi za wilaya na mkoa. Kiasi ambacho sasa ipo imani miongoni mwa wananchi wengi kuwa mipango na ahadi nyingi za viongozi wao haziwezi kutekelezwa mpaka wao wawe wamekwishakufa, yaani, kwa maneno zinachukua muda mrefu kupita kiasi na bila sababu ya kuridhsha kuwa hivyo;
. Ukubwa wa nchi daima unailazimisha serikali kufanya kazi kama zimamoto. Moto ukiwaka Dodoma leo kwa kuwa wanafunzi wa uDOM (walionekana kupatiwa kila kitu na kuridhika) wanagoma, basi ukishazimwa tu moto huo, kesho unalipuka mwingine kule Chuo Kikuu Kishirikishi cha Ardhi, Dar es salaam. Serikali inayoweza kufikia maamuzi ya mwisho pale pale mkoani ndio inayoweza kuondoa hizi kazi za zimamoto zisizokwisha.
. Ingawa wakuu wa mikoa na wilaya hawajachaguliwa na wakazi wa mkoa husika, ilivyo hivi leo ni kuwa watu hawa na viongozi wengine kama makamanda wa mikoa na maofisa mikoa wa hiki au kile huweza kujivika urais wa mkoa au wilaya kwa sababu serikali kuu iko mbali sana na wao na kile kinachoendelea mikoani au wilayani kwao;
. Fedha zikibaki Benki Kuu Dar es salaam zinaleta uroho na tamaa kwa watendaji na wanasiasa namafisadi hawachelewi kuzishughulikia kwa namna watakayo, kwa uzuri au kwa ubaya, kwa ubinafsi au kwa faida ya wengi;
. Fedha zozote zinazobaki katika kasma ya wizara za Jamhuri huko Dar es salaam ni rahisi kuvutwa na kutumika kwa mambo ambayo hazikupangiwa pale ambapo mifumo ya udhibiti ni ovyo, inayovuja saa zote na haiwezi kumuajibisha yule anayechota chochote ikiwa kama kinachochotwa ni kwa faida ya wale walioko madarakani;
. Wizara zote ziko katika kata moja jijini Dar es Salaam wakati kuna wanaoamini kwamba pasiwe na makao makuu ya wizara zaidi ya tano katika mji mmoja ikiwa tunataka kuleta uwiano katika kusambaza maendeleo kitaifa. Wanasema kama makao makuu ni Dar es salaam au Dodoma basi huko kujengwe ghorofa moja itakayohifadhi ofisi za wizara zote na ofisi hizi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ziweze kuwasiliana na makao makuu popote pale nchini kwa haraka na kirahisi kabisa katika utendaji wa shughuli zao za kila siku. Kama makao makuu ya wizara yapo Mwanza, Moshi au Mbeya basi ofisi ya Dar es Salaam/Dodoma itaitwa ofisi ndogo ya Wizara. Hivi leo (Mungu aepushie mbali) ukizuka moto pale kata ya Magogoni basi Tanzania fumba na kufumbua haitakuwa na ofisi za serikali za makao makuu ya wizara karibia zote, isipokuwa chache sana;
. Mkoa mmoja tu ndio unaofaidika na matumizi ya serikali kuu nchini na ni mkoa huo huo ndio unaonufaika zaidi kibiashara na kisiasa kuliko mikoa mingine nchini. Kusambazwa kwa wizara kama ilivyopendekezwa hapo juu kutasaidia sana mikoa mingine kunufaika pia. Wizara inapokuwa Mbeya au Kagera au Tanga ni kwamba kuna vyanzo mbalimbali vya kuwaendeleza wakazi wa huko hupatikana. Wasomi na wataalamu wa wizara hiyo wataleta mabadiko; watumishi wataongeza mzunguko wa fedha; na kazi zinazofanywa na makao ya wizara katika mkoa huu zitakuwa kivutio kwa viongozi wa kesho, yaani, watoto na vijana;
. Misongamano, foleni na utititi wa magari jijini unaendelea kukua siku hadi siku kutokana na makao makuu ya nchi kuwepo yasipostahili. Mchakato wa kuona kuwa vitongoji kando ya mji na mikoa pembezoni mwa nchi inafaa kujengwa ofisi mbalimbali za kiserikali na kwa huduma za umma kutaondoa tatizo hili haraka kuliko inavyotazamiwa;
. Magazeti yote yanachapwa kutoka Dar es salaam na matokeo yake tuna habari za ushabiki wa kisiasa zaidi kuliko habari za kimaendeleo na zile za kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi. Aidha magazeti mengi ni ya Kidaressalaamu na hayana sura yoyote muhimu ya maisha na matukio yalivyo kwenye mikoa mingine;
. Makao makuu ya redio zote kubwa ziko Dar es salaam na matokeo yake ni kama hapo juu. Hatuwezi kuzungumzia maendeleo mikoani na vijijini huku wizara zote zinashonana Dar es salaam. Ufunguo wa matatizo yetu ya mikoa na vijiji kukosa maendeleo yatapatikana kwa njia kuu mbili. Njia hizo ni Serikali Kuu kusogezwa karibu zaidi na wananchi mikoani na vijijini; na pili, ni kwa watendaji wa ngazi za chini (mikoani, wilayan, tarafani, kata na vijijini) nao kuwa wasomi na wataalamu kama wale wa ngazi za juu.
. Makao makuu yote ya vyama vya kisiasa yako Dar es Salaam, na zaidi ya chama tawala hakuna chama kingine kinachopata haki yake ya kuongoza mkoa hata kama kimeshinda katika mkoa huo. Chama tawala pekee ndicho kilicho na uwakilishi wa uhakika mikoani na vijijini, wakati vile vya upinzani vinahitaji nyenzo za kila aina kusambaa kwa kiasi hicho. Lakini kila mtu anafahamu kwamba ili mfumo wa vyama vingi ufanye kazi sawasawa ni lazima kila chama kilichopo nchini kiwe kila mahala nchini. Je, mfumo wetu na wale wanaotusaidia kukuza na kuendeleza demokrasia nchini wamekaa katika mkao wa kusaidia hili lifanyike kirahisi ? Hapana. Bado kazi ya maana haijafanyika pia katika eneo hili;
. Watumishi wengi wa serikali wanaojulikana na wasiojulikana wako Dar es salaam na wingi wao unalilemaza jiji na kukawiza maendeleo mikoani na wilayani. Kama ingelifanyika sensa ya uhitaji wa watumishi ndani ya serikali basi Dar kwa vyovyote iwavyo ingelionekana ina watumishi wasiolingana hata kidogo na kile kinachofanyika katika jiji hili ambalo sasa taka huweza kukutwa hata nyuma ya Ikulu na kuna vikojozi pembeni ya wizara kadhaa pia;
. Viwanda karibu vyote vya nchi viko katika mkoa wa Dar es Salaam na hivyo kuiacha mikoa mingine kuwa masoko ya Dar es salaam. Hili ni zuri na baya kwa upande mmoja. Kama kuna uchafuzi wa mazingira kama ule wa kule Cote d'Ivoire ni kwamba fumba na kufumbua wote tutakuwa wagonjwa na wengi kufariki kutokana na hilo. Ni zuri kwa kuwa watu wanaomiminika kuja Jijini wana nafasi kubwa zaidi ya kupata ajira na kujiendeleza kuliko wanaokwenda sehemu nyingine yoyote nchini. NI hili la pili tunalotakiwa kulisahihisha. Kwamba mtu asione anakwama kupata ajira au kujiendeleza ikiwa yuko mikoani au wilayani. Tujenge mfumo wa kiuchumi na kijamii unaowatawanya watu na watumishi mbalimbali zaidi kuliko ilivyo sasa ambapo wote wanakusanywa pamoja kwa heri au shari;
. Watalii karibu wote wasipotembelea mbuga za wanyama wanatemebela Dar es salaam. Nina hakika karibu mikoa yetu yote ina vivutio vya kitaali. Kinachokosekana ni miundo mbinu na mipango thabiti ya kufanya mikoa yote inufaike vilivyo na sekta ya utalii. Sekta inayokuwa kwa kasi zaidi kuliko nyingine yoyote nchini. Mathalani Ujiji, Kigoma ikigeuzwa kitega uchumi cha kitalii kesho na kesho kutwa tutakuwa na watalii kwenye fukwe za Ziwa Tanganyika watakaoingiza fedha kwa kuishi kwenye mahoteli au nyumba za wananchi huko; kwa kutumia vyombo mbalimbali vya usafiri vikiwemo vile vya majini (mtalii kuona zaidi ya nchi tatu akiwa KIgoma); na kwa kutembelea mbuga za wanyama za karibu na mbali. Ndivyo ilivyo kwa eneo la Maziwa ya Victoria na Nyasa pia;
. Pamoja na jitihada zote hizi kama tulivyokwishasema, serikali kuu ambayo iko Dar es salaam imeshindwa kulifanya jiji kuwa safi; maji ni tatizo; foleni barabarani asubuhi na mchana ndio kawaida; umeme hautabiriki; uhalifu na uvunjaji sheria unatawala na kadhaliika. Je, katika hali kama hii ambayo viongozi wanashindwa kulifanya jiji kuu Tanzania kuwa bora kimataifa kuna uwezekano wa viongozi hao hao kusimamia vyema mambo ya mikoa mingine ?
. Maeneo mengi ya vijijini yananaonesha ubaguzi uliopo kati ya maeneo ya mijini na yale ya vijijini ikiwemo lile la miji kupendelewa kwa huduma zote muhimu na mipango mingi ya kiserikali. Nchi yetu na viongozi wetu wakijipanga vizuri ni rahisi kwa maeneo mengi tu ya vijijini kuzalisha umeme wao, kuwa na mifumo ya maji ya bomba; na vilevile kuwa na aina ya viwanda vidogo kwa ajili ya hiki au kile kwa maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi kwa gharama nafuu zaidi kuliko kuwa na viwanda vikubwa vinavyochafua mazingira na vinavyoajiri watu wachache;
. Ipo mikoa kadhaa kama vile Iringa, Mwanza na Kilimanjaro ambayo inafanya vizuri katika masuala ya afya, usafi, mazingira na utunzaji wa miji kwa ujumla lakiji jitihada zao zinazoroteshwa na serikali kuu iliyo katika jiji ambalo sio la kuigwa katika masuala hayo. Mikoa kama hii ikipewa ruhusa ya kujiendesha huria kijamii na kiuchumi na kulilipa serikali mrabaha wake itafika mbali sana kimaendeleo katika muda mfupi sana;
. Mikoa hii itakayokuwa chini ya Waziri Mkuu na mawaziri wake wote wakiwa watu waliochaguliwa na wakazi wa mkoa husika itakuwa ni Chuo Kiikuu kwa viongozi wa serikali kuu. Haitayamkunika mtu yeyote kuja kjifunza uwaziri katika serikali kuu kabla hajapitia uwaziri mkuu katika ngazi ya mkoa. Kwa maneno mengine kuchelewesha kuwepo kwa mikoa huru kiuchumi na kijamii ni kuchelewesha maendeleo sio tu ya Tanzania nzima, bali ya Afrika na Ulimwengu, kwani yapo mengi sana dunia inayoweza kupata na kujifunza kutoka kwetu na sio sisi tu kupata na kujifunza kutoka kwa wengine.
Mikoa ingelikuwa kama Zanzibar
Fikiria mkoa wa Mwanza pembeni ya Ziwa Victoria ambao kama ungelikuwa na Waziri wake mkuu na Baraza lake la Mawaziri ungeliweza kutatua matatizo yake haraka zaidi kuliko yanavyoshughulikiwa huko Dar es Salaam. Aidha, mkoa huo ungelinufaika vilivyo na nchi jirani za Rwanda, Biurundi na Kenya kiuchumi na kijamii kuliko ilivyo hivi sasa.
Fikiria mkoa kama ule wa Mbeya au Ruvuma au Rukwa na jinsi ambavyo ungelikuwa mkoa huru ungeliweza kunufaika vilivyo na majirani zake kama Malawi, Zambia na Kongo na hususan katika kuwauzia moja kwa moja mazao ya kilimo na bidhaa nyingine na hivyo kupunguza umaskini mkubwa katika mikoa hiyo.
Wazee wetu katika zama zao waliogopa kuigawa Tanzania katika mikoa huru kwa kuhofia nchi itasambaratika. Je wamejifunza nini kutoka ile iliyokuwa ikiitwa USSR ?Jibu la hili sio gumu. Ila ukiritimba wa madaraka ukizidi (over centralization) huchangia kuisambaratisha nchi kuliko kitu kingine. Kinyume chake huko Ujerumani tumeona kwamba kugawa madaraka mikoani kunajenga umoja na mshikamano zaidi kwa nchi kuliko kinyume chake. Ona mashariki walivyorudi tena ndani ya Ujerumani moja kubwa na jinsi majimbo au mikoa huru ya Ujerumani yanavyochangia Ujerumani kuwa taifa lenye uchumi imara zaidi Ulaya kama sio duniani hivi leo.
Tunapoangalia jinsi ya kuiimarisha Tanzania ili isimezwe katika Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) jambo moja la kuzingatia ni kwamba bila mikoa huru kuwepo nchini hofu hiyo lazima itakuwa kweli tu.
Dawa ya kujiganga na hili ni kuiachia mikoa yetu mingi ambayo ni mikubwa kuliko Rwanda au Burundi kujititimua kiuchumi na kijamii ili ijenge mazingira yanayomlinda Mtanzania na kumwezesha sio tu kuhimili vishindo vya ushirikiano na nchi nyingine za Afrika Mashariki bali pia nafasi yake katika umoja wa Afrika na matatizo na fursa za nchi hii katika utandawazi na mfumo mpya wa uchumi duniani.
NInavyoona mimi, ni rahisi kwa nchi kusambaratika zaidi kwa kutegemea uongozi ulioko Dar es salaam badala ya uongozi huru ulioko mkoa husika lakini utakaowajibika katika masuala ya usalama wa ndani na ulinzi wa mipaka yake kutokea makao makuu ya nchi.
Kazi ya mkoa huru itakuwaa ni kuweka mipango ya kupambana na umaskini, ujinga, maradhi, wizi, uvivu, kukoa uwazi, kutokuwajibika, uzembe na utegeaji katika ngazi ya mkoa husika. Mkoa utashughulikia haya kwa kuwa na nguvu za juu kabisa katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiteknolojia.
Masuala ya kisiasa, kijeshi, kifedha, kiusalama na kiulinzi yataendelea kubaki mikononi mwa serikali kuu ambayo sasa italazimika kuwa na baraza dogo la mawaziri kushughulikia hasa masuala ya umoja na mshikamano wa kitaifa na kimataifa.
Hoja kwanini tuwe na mikoa huru
Kwanza, ni haki ya kikatiba kwa kila Mtanzania kupata fursa ya kuongoza na kusimamia masuala mbalimbali kwa maendeleo yake na yale ya wenzake. Kwa maneno ya baba wa taifa: " Kitendo chochote kinachomuongezea Mtanzania uhuru wa kuamua juu ya maisha yake ya kila siku ni kitendo cha maendeleo" ;
Aidha, nchi hii ni kubwa mno na haiwezi kutawaliwa moja kwa moja toka mkoa mmoja nchini. Tumeona kasheshe ya kutembelea tu baadhi ya maeneo nchini. Na hata kwa hili sehemu nyingine watu wamepita juu kwa juu wakiwa kwenye helikopta na hawakuiona kabisa hali halisi chini. Watu fulani wanaweza wakawa na tamaa ya kiukiritimba kutaka kutawala nchi toka Dar es salaam, lakini tamaa yao haina faida, tija, ufanifu wala ufanisi kwa wananchi mikoani bali inawabebesha mizigo isiyo ya lazima ambayo vinginevyo ingelitumika kuharakisha kuleta maendeleo huko mikoani;
Kwa bahati mbaya au mikoa yetu leo inategemea sana kuwa na waziri serikali au tajiri mmoja ambaye ni mbunge ili iendelee. Ukitazama matokeo ya uchaguzi mwaka huu, utaona kuwa wabunge wengi ambao walikuwa ni mawaziri au viongozi wa juu katika serikali au matajiri nchini wamerudi tena bungeni. HIli limefanyika kwa sababu wametumia baadhi ya ukwasi wao kunyunyiza maendeleo ya aina fulani katika majimbo yao ingawa katika mkoa huo huo jimbo lililoko majimbo mengine yako hoi. Hakuna kuwianisha kokote kwa maendeleo kunakofanyika na tatizo la hili huko mbele ya safari tutakuja kuwa na majimbo teule na yaliyojaliwa na majimbo ya njaa na matatizo chungu nzima. Kisiasa hii ni hatari kubwa.
Kimkoa, ina maana kwamba kama mkoa hauna mbunge ambaye ni waziri au tajiri basi maendeleo yake yatakuwa mashakani. Mtazamo wa namna hii haufai kwa kuwa utachangia kuigawa nchi na watu wake. Kuepusha hili, ni muhimu kuwa na serikali huru za mikoa zitakazowezesha eneo lote na watu wote kwa pamoja. Ugawaji wa rasilimali nchini kwa haki bila upendeleo hauwezekani kwa kutumia mfumo uliopo hivi sasa unaoongozwa toka makao makuu ya muda, Dar es salaam;
Kama Wapare, Wahaya, Wanyakyusa na Wachagga ndio waliosoma sana na wanatishia kurejesha ukabila basi hakikisha kuna sera za kunyanyua makabila yaliyobaki nyuma. Wapeleke wasiosoma kwa walisoma wakajifunze mbinu za kujikomboa. Na wawezeshe waliofunguka macho kwenda kuishi kwenye mikoa ya wasiofunguka sana macho ili kuwafungua macho na wao waendelee. Na hili litafanyika vizuri zaidi kukiwa na mikoa huru ambayo inaangalia matatizo yake na kisha kuiomba mikoa mingine kuwatumia watu inaoamini watabadilisha hali ya maisha katika mkoa husika kwa kasi ya ajabu.
Kama kuna dini ambayo watu wake wanaonekana kushika sana madaraka ya nchi basi wezesha dini nyingine nazo kuendeleza rasilimali watu ili kuleta uwiano serikalini na katika soko la ajira. Sote tunajua kuwa Waislamu wengi wako visiwani na mikoa ya Pwani na huko Bara Wakiristo ndio wengi. Kwa sera za kutawala toka Dar es salaam na kukosa mikoa huru tunaona jinsi ambavyo njaa, ujinga na maradhi yanayoongezeka katika mikoa hii kutokana na kutokuwa na serikali huru ya kimkoa inayoweza kuibua vipaji vya wakazi wake na kuwatumia wasio wenyeji kuwaendeleza na kuwajenga wenyeji;
Huwezi ukaahidi kila mkoa kulifanyia hili au lile bila kuwa na serikali thabiti ya watu iliyochaguliwa na wakazi wa mkoa husika katika kusimamia kikamilifu kupnaga, kuanzisha, kuendeleza na kudhibiti utekelezaji wa ahadi hizo ili ziwe kweli;
Kuwepo kwa Waziri Mkuu na Baraza lake la mawaziri kutaondoa ile hali ya kuwa na utitiri wa viongozi mikoani ambao wanakanyagana miguu na hawajui la kufanya ila kukubali kutumika ndivyosivyo na wale walioko madarakani;
Fursa nyingi za kimaendeleo na zile za kutatua matatizo ya wananchi mikoani na vijijini hupotea kwa sababu makao makuu Dar es Salaam hayana habari na kinachoendelea mkoani;
Mikoa huru itakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kudai mrabaha wa halali toka makampuni au migodi ya madini inayoendesha shughuli zao katika mkoa husika kuliko ilivyo kwa mangimeza wa wizara huko Dar es Salaam. Ni lazima ya Ngoswe aachiwe Ngoswe;
Matatizo yaliyopo katika suala la mawasiliano, uchukuzi, usafirishaji, menejimenti ya rasilimali watu yatajitokeza wazi zaidi panapokuwepo na mikoa huru kuliko ilivyo hivi sasa;
Utata wa baadhi ya watumishi wa umma kufanya kazi zao ipasavyo kutokana na kila kitu kusimamiwa toka makao makuu Dar es Salaam, kwa mfano kwa askari polisi mikoani, utapungua sana kama mkuu wa eneo husika atakuwepo palepale mkoani;
Kukubalika kwa mawazo ya kuwa na mfumo wa serikali unaoshabihiana na ule wa nchi nyingi zinazofanya vizuri kiuchumi leo duniani, kama vile Ujerumani, Uchina, Brazili, Afrika Kusini, Australia na kadhalika kutategemea sana wepesi wetu wa kuziweka fikra za kizamani za baadhi ya wazee wetu na wale wasio wazee sana kisiasa na kuondokana na mawazo mgando yanayoshindwa kutambua mabadiliko ya wakati wetu na nini kinachohitajika ili kututoa hapa tulipo na kutufikisha kwenye neema tunayoitafuta sasa kwa zaidi ya miaka 49. Ni muhimu wanaopinga mabadiliko haya kutambua kuwa wakati ni ukuta, na ukipigana nao utaumiza mkono wako mwenyewe.
Nani, Nini, Wapi, Kwanini, Lini na Kwa Namna Gani ndiyo maswali mapya ya enzi hizi ambayo hayataweza tena kukwepeka. Kitaifa, maswali haya yatahusu: Ni mkoa gani unapata nini na ni nani wanaopata; kwanini unapata unachokipata na sio mkoa mwingine; yatahusu pia wapi kuna rasilimali au mali asili na nani ananufaika nazo; yatakuwa juu ya kwanini mkoa fulani unapewa unachopewa na kwanini unapewa hilo katika wakati huo; yatahusu pia Lini na sisi mkoa wetu utapata, kwanini hatupati leo lakini wenzetu wanapata na ni kwa namna gani na sisi tunaweza kufikiriwa kwanza kabla ya wengine. Maswali haya yatashuka kwenye ngazi ya wilaya, tarafa, kata hata kwenye familia. Maswali kwa wanasiasa yatakuwa mengi kuliko majibu. Na wanasiasa hawataweza kuendlea kukataa kujibu maswali haya milele. Itafika wakati itabidi yajibiwe. Na kuyajibu maswali haya kutokea Dar es salaam itakuwa ni vigumu zaidi kuliko kuyajibu tokea makao makuu ya mkoa husika. HIli likiashiria kwamba maandalizi ya kuwa na mikoa huru ni vyema yaanze kufanyika kuanzia sasa, katika awamu iliyoko madarkaani vinginevyo tutakuwa tumechelewa. Na siku ya siku tutakapolazimika kuyajibu maswali hayo tutajikuta tunafungua midomo lakini hatutoi sauti....
MIKOA HURU KIUCHUMI NA KIJAMII
Blogi hii ni changamoto kwa Watanzania mikoani kudai haki ya Mikoa yao kuwa huru kiuchumi na kijamii chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haki yao kikatiba lakini mafisadi na wababya wa maendeleo yetu hawataki tuitumie kwa visingizio vya kuja kukosa amani na umoja, mambo ambayo tayari yanasababishwa na ufisadi, wizi serikali, mikataba mibovu, huduma duni na ulaji wa kutisha.
Thursday, December 30, 2010
Wednesday, September 8, 2010
Daladala 001
Sheria haziwabani abiria
Kwa macho yangu nimeshuhudia abiria kadhaa waking'ang'ania kushushwa katikati ya barabara na konda alipokaa wakamtukuna. Ninachojiuliza ni kwamba, je, konda angewashusha wale abiria na jamaa wa Majembe wakamzukia wangelikubali kuwa kosa ni la abiria na sio konda.
Ushauri ili tutende haki kwa wot lazima tuwawajibishe pia na abiria.
**************************************************************************************************************************************
Kituo cha Mwenge
Ni vizuri kama kungelijengwa vituo vingine vya daladala ili kituo cha Mwenge kipumue. Sasa hivi kila daladala hulazimika kuingia hapo na kusababisha foleni nyingine ya kipumbavu.Ninashauri pawe na kituo kingine upande wa pili ili magari yote yanayotokea njia ya Ubungo yaishie na kugeuza hapo. Na kisha pajengwe kituo cha tatu mwanzo wa kuelekea njia ya Kawe/Lugalo kwa ajili ya mabasi yanayotokea Kawe, Tegeta, Bunju na Bagamoyo. Na kituo cha sasa kibaki kwa magari yatokeayo Ali Hassn Mwinyi na Sinza tu. Turahisishie daladala uwajibikaji kwa abiria wao na tuondoe viini vya magomvi yasiyokuwa na kichwa wala mguu !
**************************************************************************************************************************************
Maktaba St. na daladala.
WAKATI umefika wa kugeuza njia ya Maktaba kuwa njia moja na isiwe njia mbili. Magari yawe yanatoka tu kuja barabara ya Bibi Titi na sio kuingia. Badala yake magari yawe yanaingilia njia ya juu kwenye nyumba ya Sanaa na Move'n'pick [Royal Palm hotel ]na hapa yawe yanaingia tu na magari yasiruhusiwe tena kutoka. Kwa kufanya hivyo, maisha ya watumia mtaa wa Maktaba yatakuwa na nafuu kubwa.
**************************************************************************************************************************************
Urahisi wa kutnga sheria, kufuatilia je ?
Kuna wakati daladala zilitakiwa kuwa na kiboksi cha 'first-aid' haraka haraka wenye mabasi walieweka viboksi hivyo. Hata hivyo, kutokana na ufuatiliaji duni daladala nyingi hivi leo hazina maboksi ya 'first-aid' na badala yake kuna viboksi vilivyogeuka takataka na hatari kwa wapanda daladala kwa jinsi vinavyoning'inia ovyo.
**************************************************************************************************************************************
Daladala zinavyokwepa wanafunzi
Inasikitisha kuona baadhi ya daladala za Tabata zinavyoruka vituo pindi waonapo mlundikano wa wanafunzi. Huu si uungwana. Waafunzi nao ni abiria na wanaostahili kuhudumiwa kama wengine. La kuchekesha zaidi utakuta daladala haina watu lakini bado inawakataa wanafunzi. Pengine nauli ya sasa ni kubwa mno kiasi ambacho shilingi mia kwa daladala nyingine haina thamani?
**************************************************************************************************************************************
Lugha chafu
Uungwana katika dalaadala sio jambo linaloonekana tena sikuhizi. Kuna watu wengine ikiwemo pia madereva na makonda wa daladala inaelekea sala yao ya kwenda kulala, ya kuamka na ile sala wakiwa barabarani ni kuomba kuomba kugombana na watu wengine. Na katika hili hakuna anayenufaika ili kujenga roho mbaya itakayowatumbukiwa Watanzania wote baada ya miaka si mingi kutoka sasa.
**************************************************************************************************************************************
Simu na madereva wa daladala
Hivi majuzi nusra tuingie lori la tani 25 lililokuwa mbele yetu eti tu kwa sababu dereva wa daladala yetu alikuwa akiongea na tajiri kuhusu sijui ushuzi gani. Hivi hao ni matajiri njaa, hugonji dereva arudishe gari ndio mzungumze au mpange siku ya dereva kupumzika ili mpange vyema yanayowahusu ?

Subscribe to:
Posts (Atom)